Taasisi ya Aqaf Trust kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kuwasaidia Wanafunzi Mkoa wa Kaskazini Unguja (JUKWAMKU), pamoja na viongozi wa Jimbo la Tumbatu, wamefanikiwa kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Pale Kirusha wadi ya kipange jimbo la Tumbatu kwa kuchimba kisima kitakachotoa huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kisima hicho, mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tumbatu, Mheshimiwa Juma Othman Hija, amesema mradi huo ni sehemu ya mikakati ya viongozi wa jimbo hilo kuhakikisha wananchi, hususan wanawake, wanapata maji safi na ya kutosha.
Amesema anaishukuru Serikali zote mbili kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya maji, na kuongeza kuwa viongozi wa jimbo hilo wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha visima vya kutosha vinachimbwa na kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi.
Aidha, Mbunge huyo ametoa shukrani kwa JUKWAMKU na wafadhili wao, Aqaf Trust, kwa kufanikisha mradi huo, na kuwataka wananchi kuyatunza maji hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Katibu wa JUKWAMKU, Soud Omar Khamis, amesema jumla ya shilingi milioni 12.5 zimetumika kukamilisha mradi huo. Ameeleza kuwa taasisi yao ina dhamira ya kusaidia jamii, na mradi huo ni sehemu ya juhudi zao za maendeleo katika mkoa huo.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana katika kutunza mradi huo, ikiwemo kuunda kamati maalum ya usimamizi ili kuhakikisha unadumu kwa muda mrefu.
Naye Diwani wa Wadi ya Kipange, Khamis Kombo Khamis Ali, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika wadi hiyo, na kupongeza juhudi za JUKWAMKU kwa kusaidia kutatua tatizo hilo.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Kirusha wamesema kabla ya mradi huo walikuwa wakipata tabu kubwa kufuata maji umbali mrefu, hali iliyowaathiri zaidi wanawake na watoto. Wameeleza kuwa mradi huo ni faraja kubwa kwao na wamewashukuru viongozi wao kwa kuwatafutia suluhisho la kudumu.
