Popular services

ACTIONAID YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI MASHULENI KUPITIA MIJADALA YA HUDUMA BORA YA MAJI NA VYOO SALAMA

 ACTIONAID YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI MASHULENI KUPITIA MIJADALA YA HUDUMA BORA YA MAJI NA VYOO SALAMA

Na Nishan Khamis, Zanzibar
Shirika la ActionAid Zanzibar limeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji mashuleni kupitia mijadala ya huduma bora ya maji na vyoo salama inayolenga kuwajengea wanafunzi mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.

Hayo yameelezwa leo katika mjadala uliofanyika katika Skuli ya Sekondari Mkwajuni kuhusu upatikanaji wa huduma ya vyoo na maji salama katika kuzuia vitendo vya udhalilishaji wa kingono shuleni.

Akizungumza katika mjadala huo, Afisa Elimu Wilaya ya Kaskazini A, Juma Mwadin Abdalla amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kupinga vitendo vya udhalilishaji mashuleni ili kuwajengea wanafunzi mazingira salama na rafiki yatakayowasaidia kufikia malengo yao ya kielimu.

Amesema uwepo wa huduma bora za maji na vyoo mashuleni una mchango mkubwa katika kuimarisha afya, usalama na heshima kwa wanafunzi sambamba na kuwajengea mazingira rafiki ya kujifunzia bila hofu ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Hussein Ali Mwinyi imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, hatua iliyosaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia nchini.

Kwa upande wake, mwakilishi wa ActionAid, Aisha Iddi Kiula amesema shirika hilo linaendesha programu hiyo katika wilaya tatu za Unguja kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi kujiamini, kutambua haki zao za msingi na kupaza sauti dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

Nao baadhi ya wanafunzi walioshiriki mjadala huo wamesema programu hiyo imechangia kuwajengea uwezo wa kujiamini, kuthubutu kueleza changamoto zinazowakabili pamoja na kuongeza usalama wao na kuimarisha mazingira bora ya kujifunzia.