Popular services

TATIZO LA UBOVU WA BARABARA MOGA MWEMBE MKALI: MKURUGENZI AFANYA ZIARA, AWAPA MATUMAINI WANANCHI

 

Mwandishi: Nishan Khamis, Moga
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Zanzibar, Mhandisi Widadi Ali Hassan, amefanya ziara katika kijiji cha Moga Mwembe Mkali, Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, kufuatia changamoto ya ubovu wa barabara ya ndani pamoja na tatizo la daraja katika kijiji hicho.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Mhandisi Widadi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na uimarishaji wa miundombinu ya barabara nchini, hivyo amewataka wananchi kuwa na subira wakati hatua mbalimbali za utekelezaji zikiendelea.
Amesema tatizo la daraja katika kijiji hicho litapatiwa ufumbuzi ndani ya mwezi huu, huku changamoto ya barabara ya ndani ikifanyiwa kazi na tayari imefikishwa serikalini kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.

Diwani wa Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Makame Machano Foum, amesema utatuzi wa changamoto hiyo utasaidia kuinua shughuli za kiuchumi na kijamii katika kijiji hicho, na kuhimiza serikali kuchukua hatua za haraka.

Kwa upande wao, wananchi wa kijiji hicho wamesema ubovu wa barabara hiyo umekuwa ukirudisha nyuma shughuli za kiuchumi na kijamii, pamoja na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wanawake hasa wajawazito wanapohitaji kufika hospitali kwa matibabu, wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka katika kutatua changamoto hiyo.