WALIMU WILAYA YA KASKAZINI A WAPEWA MAFUNZO NA TAASISI YA TARL KUTOKA KENYA KUIMARISHA UWEZO WA WANAFUNZI KUSOMA, KUANDIKA NA KUHESABU.
Na, Nishan Khamis, ZanzibarAfisa Elimu Wilaya ya Kaskazini A, Juma Mwadin Abdalla, amesema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imejipanga kuhakikisha kila mtoto wa Kizanzibari anapata elimu bora na yenye ufanisi mkubwa kwa kumwezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu ili kumjengea msingi mzuri wa maisha na maendeleo yake ya baadaye.
Afisa Elimu amesema hayo leo katika Ofisi ya Elimu Wilaya ya Kaskazini A, Mkwajuni, wakati akifungua mafunzo ya siku kumi kwa walimu wa shule za msingi kuhusu programu ya Teaching at the Right Level (TaRL) yaliyoandaliwa na taasisi ya TARL kutoka nchini Kenya kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu Zanzibar. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea walimu uwezo zaidi ili kuongeza ufanisi wa wanafunzi katika masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeendelea kuimarisha miundombinu ya elimu katika Wilaya ya Kaskazini A na Zanzibar kwa ujumla. Hata hivyo, bado ipo changamoto kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa ufanisi, jambo ambalo amesema programu hiyo itasaidia kuleta mabadiliko makubwa kwa wanafunzi hao.
Aidha, ametoa pongezi za dhati kwa taasisi ya TARL kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu katika kuimarisha sekta ya elimu Zanzibar. Pia amewanasihi walimu kuyatumia vyema mafunzo hayo ili kuleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi na kufanikisha malengo ya programu hiyo kwa manufaa ya mtoto wa Kitanzania.
Kwa upande wake, Joan Ngungi kutoka taasisi ya TARL nchini Kenya amesema ushirikiano wao na Wizara ya Elimu kupitia programu hiyo tayari umeonyesha mafanikio makubwa katika Wilaya ya Kaskazini B, hali iliyowapa hamasa ya kuendeleza programu hiyo katika Wilaya ya Kaskazini A ili kusaidia kutatua changamoto ya watoto kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu.
Nao walimu walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza programu hiyo wakisema itawaongezea ujuzi na mbinu bora za ufundishaji zitakazowasaidia kuwainua wanafunzi kitaaluma. Aidha, wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa bidii na kujituma zaidi katika kuhakikisha wanafunzi wanafikia viwango vinavyotakiwa vya elimu.
