MWANDISHI: NISHAN KHAMIS
Wananchi wa Wilaya ya Kaskazini A wametakiwa kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na maafa katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini, ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Rikizi Daniel Yussuf, wakati alipofanya ziara katika kijiji cha Eneani Donge, ambako kumekumbwa na maafa ya maji yaliyosababishwa na mvua hizo.
Katika ziara hiyo, DC Riziki amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua tahadhari, ikiwemo kuepuka maeneo hatarishi na kufuata maelekezo ya wataalamu wa maafa, huku akibainisha kuwa serikali ipo imara katika kuhakikisha hatua za haraka na za kudumu zinachukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo.
Aidha, alitoa maelekezo kwa Afisa Maafa wa wilaya hiyo pamoja na Baraza la Manispaa kuhakikisha wanaunda na kutekeleza mikakati madhubuti ya kudhibiti maji yanayotuama, ikiwemo kuboresha miundombinu ya mifereji ya maji na kuweka suluhisho la kudumu kwa maeneo yaliyoathirika.
Amesema juhudi zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, zinaendelea kulenga na kuwajali wananchi wake kwa kuhakikisha wanapatiwa huduma bora na msaada wa haraka wanapokumbwa na changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya wilaya hiyo, Adam Makame Abdulla, amesema kuwa kwa kushirikiana na maafisa wa maafa wilaya hiyo na serikali kuu watahakikisha suala hilo linafanyiwa kazi kwa muda muafaka, huku akisisitiza wananchi kutunza mazingira na kuchukua hatua stahiki za maafa pindi yanapotokea.
Naye mkazi wa kijiji cha Eneani Donge, Seif Khatib Seif, amepongeza juhudi za viongozi hao kwa kufika katika eneo hilo na kujionea hali halisi, akieleza kuwa hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto hiyo, huku akiomba hatua za haraka zichukuliwe hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika.
