Popular services

JUMUIYA YA WAZAZI CCM KIWENGWA YAADHIMISHA SIKU YAO KWA USAFI KITUO CHA AFYA UPENJA,DIWANI ATOA WITO.

 

Mwandishi: Nishan Khamis, Upenja
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wadi ya Kiwengwa leo imeadhimisha siku yao kwa vitendo kwa kufanya zoezi la usafi katika Kituo cha Afya Upenja, Wilaya ya Kaskazini B, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mazingira bora ya huduma za afya kwa jamii.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wadi ya Kiwengwa, Alli Kwaza Nyendo, amesema maadhimisho hayo yamelenga kuhamasisha wanajumuiya na wananchi kwa ujumla kushiriki katika shughuli za maendeleo, hususan usafi wa mazingira. Amesisitiza kuwa usafi ni msingi wa afya bora na unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya kila mwananchi.

Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Kiwengwa, Mtumwa Juma Mshamba, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza usafi wa mazingira, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama kwa wananchi.

Aidha, Diwani huyo ametoa wito kwa wananchi kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi mara kwa mara na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii ili kudumisha afya na ustawi wa jamii.

Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya hiyo waliopata nafasi ya kuzungumza wamesema zoezi hilo limekuwa na manufaa makubwa kwa jamii, huku wakiahidi kuendelea kushiriki katika shughuli kama hizo ili kuimarisha maendeleo katika eneo lao.