Popular services

DC RIZIKI ATOA ONYO KALI KWA WAMILIKI WA BAA NA KUMBI ZA STAREHE WANAOKIUKA KANUNI NA SHERIA ZA NCHI.

 DC RIZIKI ATOA ONYO KALI KWA WAMILIKI WA BAA NA KUMBI ZA STAREHE WANAOKIUKA KANUNI NA SHERIA ZA NCHI.

Mwandishi:Nishan Khamis, Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kaskazini A ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Riziki Daniel Yussuf, amewataka wamiliki wa baa na kumbi za starehe katika wilaya hiyo kufuata sheria, kanuni na taratibu za biashara hizo kwa kuheshimu mila na silka za Kizanzibari pamoja na kuepuka kuwapa usumbufu wananchi wanaoishi jirani na maeneo yao.

Mheshimiwa Riziki amesema hayo leo katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Manispaa ya Wilaya hiyo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kufuatia operesheni iliyofanywa katika baa ya Pwani Vanilla House iliyopo Pwani Mchangani, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo hilo kuhusu ukiukwaji wa sheria na maadili ya utamaduni wa Kizanzibari.
Amesema kuwa watuhumiwa 13 wamefikishwa katika Kituo cha Polisi Mkokotoni kwa hatua zaidi za kisheria.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa wamiliki wa kumbi za starehe kuzingatia sheria za nchi, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria hizo. Pia ameipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na jamii kwa ujumla kwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa sheria na kanuni ndani ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Sanaa Zanzibar, Chumu Juma Chumu, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya sanaa nchini, hivyo haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wamiliki wa kumbi za starehe na watu wengine wanaokiuka sheria na taratibu zilizowekwa, kwa lengo la kuendelea kulinda mila na silka za Kizanzibari.

Aidha, amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wataendelea kushirikiana naye katika juhudi mbalimbali za maendeleo wilayani humo, sambamba na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi.