Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwaelimisha watoto kuhusu namna ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji vinavyoendelea kujitokeza katika jamii, akieleza kuwa malezi bora ndiyo nguzo muhimu ya kuandaa kizazi chenye heshima, nidhamu na uwajibikaji.
Mhe. Tamima amesema hayo leo katika kijiji cha Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhi Qur’an ya kijiji hicho.
Amesema jamii ina wajibu mkubwa wa kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanapata elimu ya dini pamoja na maadili yatakayowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuziunga mkono taasisi za dini zinazojishughulisha na malezi ya vijana.
Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kuendelea kuwafuatilia watoto wao kwa karibu, kuwapa malezi bora na kuwajengea mazingira salama yatakayowasaidia kukua katika misingi ya dini, heshima na uzalendo.
Awali akisoma risala katika hafla hiyo, Ustadhi Kali Haji Mcha amesema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kusimamia na kuwaelimisha vijana hao kuhusu kuhifadhi Qur’an Tukufu, bado jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo yake.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa vifaa na vitendea kazi muhimu kwa ajili ya kufundishia, uchache wa mfuko wa jumuiya katika kuendesha shughuli za dini pamoja na uhaba wa rasilimali zinazohitajika katika kuimarisha shughuli za malezi na elimu ya Qur’an.
Kutokana na hali hiyo, ameomba serikali, viongozi, taasisi za maendeleo na watu wenye uwezo kujitokeza kusaidia juhudi za jumuiya hiyo ili kuimarisha mazingira bora ya utoaji wa elimu ya dini kwa watoto na vijana.
Kwa upande wao wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo wametoa pongezi za dhati kwa Mhe. Tamima Haji Abbas kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi na kuunga mkono shughuli za kijamii na kidini zinazolenga kuimarisha maadili na ustawi wa jamii.
Wamesema mchango wake katika maendeleo ya jamii pamoja na ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za kijamii ni kielelezo cha uongozi unaowajali wananchi na unaochochea maendeleo endelevu katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
