Mwandishi:Nishan Khamis, Zanzibar.
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma amewasisitiza wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuendelea kushirikiana na viongozi mbalimbali katika kuharakisha maendeleo ya mkoa huo pamoja na taifa kwa ujumla.
Dkt. Riziki amesema hayo leo alipoungana na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa huo, Shadya Haji Omar, katika ziara ya kukutana na wanawake wa mkoa huo sambamba na wajumbe wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Kaskazini Unguja. Hafla hiyo imefanyika katika Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinaendelea kuthamini mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo ya taifa. Amesema lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuunga mkono juhudi za viongozi wa nchi katika kuwatumikia wanawake katika nyanja mbalimbali.
Dkt. Riziki amesema wanawake ni nguzo muhimu ya maendeleo ya chama na taifa, hivyo kuna haja kwao kuendelea kuwa mstari wa mbele katika shughuli za maendeleo, kudumisha mshikamano pamoja na kuunga mkono juhudi za viongozi wa nchi.
Aidha, ametoa wito kwa wanawake hao kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na kukipambania Chama Cha Mapinduzi ili kuongeza nguvu katika kuijenga jamii yenye maendeleo na ustawi.
Katika hafla hiyo, Dkt. Riziki Pembe Juma na Shadya Haji Omar wamekabidhi vifaa mbalimbali kwa makatibu wa majimbo ya UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, vikiwemo meza na viti kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao. Pia wametoa fedha taslimu pamoja na sadaka ya nyama yenye zaidi ya kilo 486 kwa wanawake zaidi ya 200 wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kufuatia siku za Eid Al-Adha.
Kwa upande wake, Shadya Haji Omar amesema wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wanapaswa kuendelea kuwa wamoja na kushirikiana katika kuendeleza shughuli za maendeleo pamoja na kuimarisha Umoja wa Wanawake Tanzania.
Amesema wataendelea kuwa karibu na wanawake hao ili kuhakikisha wanapata fursa mbalimbali za maendeleo sambamba na kuendeleza mshikamano ndani ya chama na jamii kwa ujumla.
Nao baadhi ya wanawake wa Mkoa huo wamewashukuru viongozi hao kwa kuendelea kuwajali na kuwapatia misaada mbalimbali inayogusa maisha yao ya kila siku, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuimarisha maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.
