Popular services

 Mwandishi: Nishan Khamis, Kidombo

Diwani wa Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Makame Machano Foum ameendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara kwa wanawake wajasiriamali katika skuli mbalimbali za wadi hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya diwani huyo kushusha vifusi na kushirikiana kwa karibu na wanawake hao katika ujenzi wa baraza maalum la biashara litakalowasaidia kufanya shughuli zao katika mazingira bora, salama na yenye kuzingatia afya za wanafunzi pamoja na wafanyabiashara wenyewe.

Akizungumza katika eneo hilo, diwani huyo alisema kuwa maendeleo ya wananchi yanahitaji ushirikiano na vitendo, huku akisisitiza kuwa wanawake ni sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa jamii hivyo wanahitaji kuwekewa mazingira rafiki ya kujiongezea kipato.

Aidha amesema kuwa ataendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora pamoja na mazingira yanayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Sambamba na hilo, diwani huyo ameendelea kumwaga vifusi katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Mkwajuni ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na kurahisisha shughuli za wananchi katika maeneo tofauti ya jimbo hilo.

Pia aliwashukuru wawekezaji na wadau wa maendeleo wanaoendelea kushirikiana na viongozi wa jimbo hilo katika kusaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Kwa upande wao, wanawake wajasiriamali wa Wadi ya Kidombo wamempongeza diwani huyo kwa moyo wake wa kujitolea na namna anavyoshughulikia changamoto zao kwa vitendo.

Walisema tangu kuingia kwake madarakani ameendelea kuwa karibu na wananchi, kusikiliza matatizo yao na kutafuta suluhisho kwa wakati jambo ambalo limeongeza matumaini kwa wananchi wa eneo hilo.

Wanawake hao walieleza kuwa Makame Machano Foum ni kiongozi wa watu mwenye kujali wananchi wake pamoja na maendeleo yao, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana naye katika kulinda na kuendeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wadi hiyo.