Popular services

 Mwandishi: Nishan Khamis, Matemwe.

Familia za koo tatu za Kachongwa, Matemwe, leo zimetoa msimamo mkali dhidi ya mtu au kikundi chochote kinachodaiwa kuwa na njama za kuuza sehemu ya mava iliyopo eneo la Kisima Ndizi, Shehia ya Matemwe Kaskazini, wakisisitiza kuwa eneo hilo ni maalum kwa ajili ya maziko na halipaswi kutumika kwa shughuli nyingine yoyote.

Msimamo huo umetolewa katika kikao maalum cha familia hizo kilichofanyika leo kwa lengo la kulinda na kuhifadhi eneo hilo ambalo wameeleza kuwa ni urithi wa kihistoria uliopo tangu enzi za mababu zao.

Mbali na kupinga vikali suala la uuzwaji wa eneo hilo, familia hizo pia zimekubaliana kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga pamoja na utupaji wa taka katika eneo la makaburi, huku zikionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka maamuzi hayo.

Katika kikao hicho, wajumbe wa familia hizo walieleza kuwa kumekuwa na taarifa zinazoashiria kuwepo kwa baadhi ya watu wanaotaka kuuza eneo hilo, jambo walilolieleza kuwa ni kosa na kinyume na makubaliano ya ukoo pamoja na matumizi halali ya eneo hilo ambalo limekuwa likitumika kwa maziko tangu enzi za mababu zao.

Akizungumza katika kikao hicho, Sheha wa Shehia ya Matemwe Kaskazini, Wadi Ali Wadi, amesema maamuzi yaliyofikiwa lazima yaheshimiwe na kusimamiwa kwa nguvu zote, huku akisisitiza kuwa sheria zitachukua mkondo wake kwa yeyote atakayokwenda kinyume na makubaliano hayo.

Sheha huyo pia alizipongeza familia za koo tatu za Kachongwa kwa kuandaa kikao hicho na kufikia maamuzi ya pamoja kuhusu kulinda eneo hilo la mava, akieleza kuwa mshikamano wao ni hatua muhimu katika kuhifadhi urithi, mila na utamaduni wa jamii hiyo.

Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Kijini, Faki Zuber Haji, alisema ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha eneo hilo linaendelea kubaki kuwa sehemu maalum ya mava pekee. Pia aliwataka wananchi kuacha vitendo vya uharibifu wa mazingira katika eneo hilo na kushirikiana katika kulinda maeneo ya kihistoria na kijamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.