KATIBU TAWALA MKOA NA WILAYA KASKAZINI B WAAPISHWA, RC GALLOS ASISITIZA USHIRIKIANO NA KUDHIBITI UKIUKWAJI WA SHERIA KATIKA KUMBI ZA STAREHE.
Mwandishi:Nishan Khamis, Zanzibar.Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Gallos Nyimbo, leo amewaapisha Makatibu Tawala wa ngazi ya mkoa huo pamoja na Wilaya ya Kaskazini B, kufuatia uteuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, wenye lengo la kuimarisha safu ya viongozi wa mkoa na wilaya katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Akitoa nasaha, Mhe. Gallos amesema maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja yanahitaji mshikamano, uwajibikaji na ushirikiano wa pamoja baina ya viongozi na wananchi ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati na ufanisi zaidi. Amesisitiza viongozi hao kufanya kazi kwa karibu na wananchi pamoja na kusimamia maadili ya utumishi wa umma kwa maslahi ya taifa.Aidha, amesema mkoa huo unaendelea kuwa salama na tulivu kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi. Ameeleza kuwa hali hiyo imechangia kuimarika kwa shughuli za kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Sambamba na hilo, ametoa pongezi za dhati kwa viongozi wa wilaya pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama kwa kuendeleza ushirikiano mzuri katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano ndani ya mkoa huo.
Akitoa neno la shukrani, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ameir Ali Haji, amesema wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano na uzalendo mkubwa kwa maslahi ya wananchi na taifa, huku wakiahidi kwenda sambamba na maelekezo ya viongozi wakuu wa serikali katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi zaidi.
Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa pamoja na wadau tofauti wa maendeleo walihudhuria kushuhudia tukio hilo muhimu.
