Popular services

 Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, amesema kuwa mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini yaliyofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar yana malengo mazuri ya kuwapatia wanafunzi elimu bora yenye tija baada ya kumaliza masomo yao.


Amesema mitaala hiyo inalenga kuwawezesha wanafunzi kujitegemea na kujiajiri, hususan katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii na lugha za kigeni.

Ameongeza kuwa Wilaya ya Kaskazini A imezungukwa na shughuli nyingi za kitalii, hivyo ni fursa kwa wanafunzi kutumia vyema elimu wanayoipata kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Meya huyo ameyasema hayo leo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha nne mwaka 2025 yaliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Matemwe, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi, walezi na walimu kushirikiana kwa karibu katika kuwasimamia wanafunzi ili kuongeza ufaulu wa kitaaluma. Pia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mila na silka za Kizanzibari, hususan katika ukanda wa Matemwe, ili kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Makame Sheha, ametoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Husein Ali Mwinyi, kwa juhudi zake katika kuimarisha miundombinu ya elimu kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, hatua ambayo imeleta mabadiliko chanya katika skuli hiyo.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa madarasa ukilinganisha na idadi ya wanafunzi, upungufu wa walimu katika baadhi ya masomo, pamoja na matatizo ya miundombinu ya kielimu. Ameiomba serikali kupitia wizara husika kushughulikia changamoto hizo ili kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Naye mwanafunzi Tatu Khamis Moss, akisoma risala katika hafla hiyo, amesema miongoni mwa mafanikio ya skuli hiyo ni kupungua kwa daraja sifuri katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia. Hata hivyo, ameeleza kuwa uhaba wa walimu bado ni changamoto kubwa inayohitaji kutatuliwa.