Na Nishan Khamis, Zanzibar
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Daniel Yussuf, kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, wamefanya operesheni maalum ya kushtukiza usiku katika bar ya Pwani Vanilla House iliyopo Shehia ya Pwani Mchangani, Wilaya ya Kaskazini A.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu usumbufu uliokuwa ukitokea katika eneo hilo, ikiwemo ukiukwaji wa sheria na baadhi ya wanawake kucheza muziki wakiwa katika mavazi yasiyoendana na maadili na utamaduni wa Kizanzibari.Amesema katika operesheni hiyo jumla ya watu 13 walikamatwa, wakiwemo wanawake 11 na wanaume 2, na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Mkokotoni kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Mhe. Riziki ametoa onyo kali kwa wamiliki wa baa na sehemu za starehe katika wilaya hiyo kuhakikisha wanaendesha biashara zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya nchi, huku akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachokiuka utaratibu uliowekwa.
Aidha, amepongeza juhudi za Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wao katika kupambana na vitendo vinavyokiuka maadili na kuhatarisha usalama wa jamii.
Kwa upande wake kamishina wa utamaduni Zanzibar, Dkt Omar Salum Mohamed amesema kuwa baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, hususan wanawake, kuhusu ukiukwaji wa sheria, kanuni na mila za Kizanzibari katika bar hiyo, waliamua kufanya operesheni hiyo maalum ili kuhakikisha sheria zinafuatwa na hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wahusika.
Dkt. Omar ameonya kuwa Zanzibar ina mila, desturi na utamaduni wake unaopaswa kuheshimiwa, na kwamba yeyote atakayekiuka sheria na maadili ya jamii atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.
