Popular services

VIONGOZI MKWAJUNI WAFANYA ZIARA YA MAENDELEO, WAKABIDHI MATOFALI, MIPIRA YA MAJI NA TELEVISHENI.

 

Na,Nishan khamis, Mkwajuni.
Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, Mheshimiwa Khamis Ali Vuai, leo ameongoza ziara maalum na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo kwa lengo la kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa khamis amekabidhi matofali mia nne katika Skuli ya Msingi Kibuyuni kwa ajili ya ujenzi wa banda la kukalia watu pamoja na jiko, Aidha, ametoa mipira ya maji katika kijiji cha Chutama ili kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama.

Vilevile, mbunge huyo amekabidhi televisheni kwa vijana wa Maskani ya Mkungu Yanga, hatua inayolenga kuwawezesha vijana hao kujihusisha na shughuli za kijamii. Pia alimtembelea na kumfariji mwananchi wa kijiji cha Kibeni aliyepata maafa  baada ya nyumba yake kubomoka kufuatia mvua.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mheshimiwa Vuai amesema jumla ya shilingi milioni 2.9 zimetumika kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo, na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuziwasilisha serikalini kwa ufumbuzi zaidi.

Nae diwani wa wadi ya kidombo  Makame Machano Fumu amesema ataendelea kushirikiana ipasavyo na wananchi na kuchukua changamoto zao na kukaa na viongozi wenzake kwa ajili ya kutatua changamoto izo huku akiwanasihi kuendelea kutunza amani na utulivu nchini

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Jimbo la Mkwajuni, Juma Mshenga Juma, amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, akibainisha kuwa bado kuna changamoto ya maji hususan katika kijiji cha Kibeni.

Nao wananchi wa jimbo hilo, wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamepongeza juhudi za viongozi wao na kuwataka kuendeleza kasi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya jimbo.