Popular services

 Mwandishi: Nishan Khamis

Nungwi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja imesema itaendelea kushirikiana na wawekezaji na kutambua mchango wao mkubwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi ndani ya mkoa huo kupitia uwekezaji mbalimbali unaofanyika
.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, katika hafla ya ufunguzi wa duka kubwa la kampuni ya Yas, amesema uwekezaji huo una mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya mkoa pamoja na kuongeza pato na kutoa ajira kwa vijana.
Mstahiki Meya amewahakikishia wawekezaji kuwa mkoa huo upo salama na umejipanga kuendelea kushirikiana nao kwa maslahi mapana ya maendeleo. Aidha, amewapongeza kwa kuona umuhimu wa kufungua duka kubwa katika mkoa huo wenye shughuli nyingi za kitalii, hatua ambayo itasaidia kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi na watalii.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wageni wanaotembelea mkoa huo.
Pia amesema Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kukuza maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mtandao wa Yas Tanzania, Bi. Mwangaza Matatola, alisema kampuni hiyo imeamua kufungua duka hilo kutokana na ongezeko kubwa la watumiaji wa mtandao huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambao kwa kiasi kikubwa umezungukwa na shughuli za kitalii.
Alisema uwepo wa duka hilo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kuwafikia karibu zaidi wateja wake kwa kuwapatia huduma zote muhimu kwa haraka na ufanisi.

Bi. Matatola pia alitoa pongezi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano walioutoa katika kufanikisha uwekezaji huo wenye lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wao, wananchi wa eneo hilo wamepongeza hatua ya kufunguliwa kwa duka hilo, wakisema hapo awali walilazimika kufuata huduma mbalimbali mjini jambo lililokuwa likiwasababishia usumbufu mkubwa.
Wamesema uwepo wa huduma hizo karibu utarahisisha shughuli zao za kila siku na kuahidi kuendelea kushirikiana na kampuni hiyo katika kuleta maendeleo zaidi ndani ya mkoa huo.