Mwandishi: Nishan Khamis
Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC) imeendesha zoezi la utoaji elimu kuhusu haki za binadamu kwa wanafunzi wa shule za sekondari Ramadhan Haji Faki iliyopo Gamba na Mkwajuni, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uelewa wa kisheria mashuleni.
Zoezi hilo ni sehemu ya kampeni za uhamasishaji wa kisheria kuhusu haki za binadamu, huduma za haki na kuzuia vitendo vya vurugu katika muktadha wa baada ya uchaguzi, chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kupitia mradi wa LEAP II.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A, Asia Fadhil Makame, amesema lengo la programu hiyo ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa haki zao za msingi pamoja na kuwasaidia kujua njia sahihi za kuzidai pindi zinapovunjwa.
Amesema elimu hiyo pia inalenga kuwajenga vijana kuwa raia wanaojitambua kisheria, wanaoweza kuepuka vitendo vya udhalilishaji, vurugu na migogoro isiyo ya lazima katika jamii.
Salma Ibrahim kutoka NAPAC akiwasilisha mada kwa wanafunzi hao, amesisitiza kuwa elimu ya haki za binadamu ni muhimu kwa kila mwanafunzi na jamii kwa ujumla, kwani inawasaidia kujua haki zao, kuwalinda dhidi ya ukatili na kuwa mabalozi wa amani.
Ameongeza kuwa uelewa wa haki hizo unachangia kupunguza migogoro mashuleni na kuwajengea wanafunzi ujasiri wa kutafuta haki kwa njia sahihi za kisheria.
Wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza NAPAC kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuifanyia kazi, pamoja na kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha haki, amani na nidhamu kwa wenzao.
Mradi wa LEAP II unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuimarisha uelewa wa kisheria kwa vijana na jamii, hususan katika masuala ya haki za binadamu na kuzuia vurugu.
