Popular services

MSTAHIKI MEYA NYANGE AWAPA SOMO WANAFUNZI WA MLIMANI MATEMWE KATIKA HAFLA YA MAHAFALI YA KIDATO CHA NNE SKULI HIYO.

 

Na,Nishan khamis, Matemwe.
Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A na Diwani wa Wadi ya Gamba, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, leo ameongoza mamia ya wananchi, walimu na wanafunzi katika mahafali ya nne ya kidato cha nne ya mwaka 2025 yaliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Mlimani Matemwe.

Hafla hiyo iliyogubikwa na shamrashamra, furaha na matumaini kwa wahitimu, imekuwa jukwaa muhimu la kusisitiza nafasi ya elimu katika kujenga maisha bora ya vijana na maendeleo ya taifa.
Akitoa hotuba yake kama mgeni rasmi, Mheshimiwa Nyange alisisitiza kuwa elimu ni msingi muhimu unaoweza kumbadilisha mtu na jamii kwa ujumla.
Amewataka wanafunzi kutambua thamani ya elimu waliyoipata, kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kutokukata tamaa katika safari yao ya kutafuta maarifa.
Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya elimu nchini, ikiwemo kuboresha miundombinu ya skuli, kuongeza walimu na kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Meya aliwataka wazazi na walezi kuongeza ushirikiano na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata malezi bora pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa masomo yao.

Kwa upande wake, mwalimu Khalid Abdillah Iddi, akisoma risala ya skuli, alieleza kuwa licha ya mafanikio yanayopatikana, bado skuli inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ushirikiano mdogo wa baadhi ya wazazi, uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, ukosefu wa ukumbi mkubwa wa mikutano pamoja na uhitaji wa uzio wa skuli kwa ajili ya kuimarisha usalama.

Aidha, aliiomba serikali na wadau mbalimbali wa elimu kusaidia kutatua changamoto hizo ili kuinua zaidi kiwango cha elimu katika skuli hiyo.

Naye mwanafunzi Ruwaida Hemed Mohammed, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wahitimu, alieleza kuwa mafanikio yao yametokana na juhudi kubwa za walimu pamoja na msaada wa wazazi wao. Alisisitiza kuwa wahitimu wako tayari kutumia maarifa waliyopata kuitumikia jamii na taifa kwa ujumla.

Mahafali hayo yameacha alama ya matumaini kwa wahitimu huku yakitoa ujumbe mzito kwa jamii juu ya umuhimu wa ushirikiano katika kuinua sekta ya elimu.