Mwandishi: Nishan Khamis, Mkwajuni
Zanzibar Petroleum Development Company (ZPDC) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha jamii inaelewa vyema umuhimu wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa taifa.Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha mabalozi na wajumbe wa Shehia ya Mkwajuni, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa kampuni hiyo, Walid Moh'd Adam amesema elimu hiyo inalenga kujenga uelewa sahihi kwa wananchi kuhusu hatua mbalimbali za utafutaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na faida zinazoweza kupatikana kupitia rasilimali hizo.
Amesema ushirikishwaji wa wananchi ni jambo muhimu katika kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa uwazi, usalama na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wa Zanzibar. Aidha, amewataka mabalozi na wajumbe hao kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii katika maeneo yao ili kuondoa dhana potofu zinazoweza kujitokeza kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia.
Kwa upande wao, mabalozi na wajumbe wa Shehia ya Mkwajuni wameishukuru ZPDC kwa kutoa elimu hiyo wakisema imewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu shughuli za mafuta na gesi asilia pamoja na mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
wamesema mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya kuhusu namna rasilimali za mafuta na gesi zinavyoweza kusaidia kuongeza ajira, kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kijamii endapo zitasimamiwa vizuri. Pia wameitaka ZPDC kuendelea kutoa elimu mara kwa mara ili wananchi wengi zaidi waweze kuelewa na kushiriki katika maendeleo ya sekta hiyo muhimu.
