Popular services

 Mwandishi: Nishan Khamis, Mkwajuni

Jamii imetakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pamoja na vikundi vya ulinzi shirikishi katika kupambana na vitendo vya kihalifu na udhalilishaji nchini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Polisi jamii Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi Mussa Seif Gumbo, akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi wa mkoa huo, walipokuwa wakizungumza na wajumbe pamoja na mabalozi wa Shehia ya Mkwajuni katika kikao cha pamoja kilicholenga kutokomeza vitendo vya udhalilishaji na uhalifu sambamba na kuimarisha ulinzi shirikishi katika shehia hiyo.

Amesema jamii ina wajibu wa kutoa ushirikiano katika kuwabaini wahalifu na kupinga vitendo vya udhalilishaji, wizi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ili kuendeleza uwepo wa amani na utulivu katika shehia hiyo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na  Ulinzi wa Watoto Mkoa wa Kaskazini Unguja, Inspekta Salum Khamis Machano, amesema jitihada za pamoja zinahitajika katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji mkoani humo.

Aidha, amewataka wananchi kuripoti vitendo hivyo na kuwa mstari wa mbele katika kutoa ushahidi wa kesi hizo badala ya kufanya muhali, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya udhalilishaji nchini.

Amebainisha kuwa jamii ikiacha tabia ya muhali na kutoa ushirikiano kwa kuripoti kesi hizo katika vyombo husika, hatua hiyo itasaidia kupunguza na hatimaye kuondoa vitendo vya udhalilishaji katika mkoa huo.

Naye Diwani wa Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Makame Machano Fumu, akizungumza katika kikao hicho, amesisitiza wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu kwani ni kosa kisheria na huwanyima haki zao za msingi kama wananchi wengine.

Amesema ushirikiano wa wazazi na walezi unahitajika katika malezi bora ya watoto.

Nao baadhi ya wananchi walioshiriki kikaoni hapo wamesema bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kuhusu udhalilishaji. Aidha, wameeleza kuwa ukosefu wa vyombo maalumu vya kushughulikia kesi za udhalilishaji ni changamoto inayorudisha nyuma juhudi za kupambana na vitendo hivyo. Hivyo wamependekeza kuwepo kwa doria za mara kwa mara ili kuimarisha usalama na kuondoa vitendo vya kihalifu katika shehia hiyo.