DC RIZIKI: HATUA KALI ZITACHUKULIWA DHIDI YA WATAKAO BAINIKA KUTUMIA BANDARI ZISIZO RASMI KUSAFIRISHA ABIRIA WILAYA YA KASKAZINI A.
Na Nishan Khamis, Zanzibar.Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Daniel Yussuf, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama, wasimamizi wa bandari pamoja na jamii kwa ujumla kushirikiana ipasavyo katika kudhibiti matumizi ya bandari zisizo rasmi katika wilaya hiyo.
DC Riziki amesema hayo leo katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Manispaa Mkokotoni, wakati wa kikao maalum kilichowakutanisha wadau wa bandari, masheha, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na kamati za uvuvi, kwa lengo la kujadili na kupanga mikakati madhubuti ya kudhibiti athari zitokanazo na matumizi ya bandari zisizo rasmi katika wilaya hiyo.
Amesisitiza kuwa bado kuna uwepo wa bandari zisizo rasmi ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa nchi pamoja na kukosesha taifa mapato kutokana na shughuli zinazofanyika katika bandari hizo. Hivyo, ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana katika kuimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo kwa maslahi ya kudumisha amani, ulinzi na usalama wa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Zanzibar Maritime Authority(ZMA) Bandari ya Mkokotoni, Simai Nyange Simai, amesema kuwa licha ya hatua za utoaji wa faini za papo kwa papo kwa wanaokiuka kanuni na taratibu za ZMA, bado kuna changamoto ya baadhi ya vyombo vya usafiri kusafirisha abiria kupitia bandari zisizo rasmi katika wilaya hiyo.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa tathmini, zaidi ya watu 80 hupoteza maisha baharini kila mwaka kutokana na matumizi ya njia zisizo salama, hivyo ametoa wito wa kuongezwa kwa udhibiti wa bandari hizo kwa maslahi mapana ya usalama wa jamii na taifa kwa ujumla.
Nao baadhi ya masheha, wadau pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama walioshiriki kikao hicho wamesema kuwa ushirikiano wa karibu unahitajika katika kudhibiti vitendo hivyo, ikiwemo kupambana na uhamiaji haramu, kuzuia uingizaji wa dawa za kulevya pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato ya taifa katika wilaya hiyo.
Aidha, wametoa wito wa kuondoa muhali katika utekelezaji wa sheria na kuimarisha usimamizi wa maeneo yote yanayotumika kinyume cha utaratibu rasmi.
