Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Riziki Daniel Yussuf, amewataka madiwani wa wilaya hiyo kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao, kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato, kuimarisha ulinzi na usalama katika mipaka ya wilaya, pamoja na kudumisha usafi wa mazingira ili kuendelea kuvutia watalii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuandaa na kutekeleza miradi yenye tija pamoja na kuanzisha programu maalumu za kuwawezesha vijana kiuchumi ili kuongeza fursa za ajira na kujitegemea.
Mheshimiwa Riziki ameyasema hayo leo wakati akitoa nasaha zake katika Kikao cha Nne cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Manispaa Mkokotoni, kwa ajili ya kujadili na kutathmini utekelezaji wa shughuli za baraza kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa wilaya hiyo , Adam Abdalla Makame, amesema manispaa imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia sheria na miongozo mbalimbali, hususan katika sekta za usafi wa mazingira na ukusanyaji wa mapato.
Amesema Wilaya ya hiyi miongoni mwa maeneo yanayotegemea zaidi sekta ya utalii kama chanzo kikuu cha mapato, hivyo kuna ulazima wa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote na mapato yanakusanywa kwa ufanisi kwa manufaa ya wilaya na Zanzibar kwa ujumla.
Aidha,ametoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha usafi wa mazingira na kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi na tozo mbalimbali za kisheria katika maeneo yao ya biashara. Ameeleza kuwa asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa hutengwa kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa mikopo wa asilimia 10.
Kwa upande wao, madiwani waliowasilisha ripoti za Kamati ya Afya ya Jamii na Mazingira pamoja na Kamati ya Sheria, wamesema kuna umuhimu wa kufanya ziara za mara kwa mara za ukaguzi na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Wamesisitiza kuwa usimamizi mzuri wa sheria, usafi wa mazingira na ukusanyaji wa mapato ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya wilaya, huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika juhudi zake za kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi.
