Popular services

WANANCHI NUNGWI WATAKIWA KUEPUKA KUTUMIA BANDARI ZISIZO RASMI KATIKA KUSAFIRISHA ABIRIA.

 

Mwandishi, Nishan khamis Zanzibar.

Serikali ya Wilaya ya Kaskazini A imeendelea kuhamasisha wananchi kufuata sheria na taratibu za usafiri wa baharini kwa kuepuka matumizi ya bandari zisizo rasmi, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa afya za wananchi, kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu na kulinda mipaka ya nchi.Wito huo umetolewa leo  katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika Skuli ya Msingi Nungwi wilaya ya kaskazini A .

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa ZMA Kaskazini Unguja, Simai Nyange Simai, amesema kuwa kampeni hiyo ni mwendelezo wa juhudi za kuielimisha jamii juu ya madhara ya kutumia bandari zisizo rasmi ikiwemo bandari ya Nungwi.
Amesema matumizi ya bandari hizo yanaweza kuchangia kuingia kwa magonjwa hatari ya kuambukiza kama Ebola, kuingiza wahamiaji haramu pamoja na kurahisisha shughuli za usafirishaji ambazo hazijapewa mamlaka rasmi, ameonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wake, Afisa wa Afya wilaya hiyo , Khamis Haji Khatib, amesema kuwa bandari zisizo rasmi ni moja ya njia zinazoweza kuchangia kuenea kwa magonjwa mbalimbali ya kuambukiza. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kufuata taratibu rasmi za usafiri ili kulinda afya zao na jamii kwa ujumla.

Nahodha Mkuu wa KMKM Nungwi, Makame Kassim Haji, amesema kuwa wananchi wanapaswa kuheshimu sheria na kanuni zilizowekwa, huku akibainisha kuwa KMKM itaendelea kuimarisha doria za mara kwa mara baharini ili kuzuia magendo na kulinda mipaka ya nchi. Ameongeza kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu hizo.

Masheha wa Shehia za Nungwi Bandakuu, Kiungani na Kilindi wamewataka wananchi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa kwa ajili ya usalama wa shehia zao, wilaya na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, wamiliki wa vyombo vya usafiri na wavuvi wa Nungwi, Khatib Mohammed Khatib na Mbarawa Sheha Ali, wameahidi kutii agizo hilo na kuwa mabalozi wa kuelimisha wengine kuhusu umuhimu wa kutumia bandari rasmi.