Popular services

VITONGA VYATAJWA KUCHOCHEA ONGEZEKO LA MALARIA, KESI 46 ZARIPOTIWA KASKAZINI A, NUNGWI YAONGOZA KWA MAAMBUKIZI.

 VITONGA VYATAJWA KUCHOCHEA ONGEZEKO LA MALARIA, KESI 46 ZARIPOTIWA KASKAZINI A, NUNGWI YAONGOZA KWA MAAMBUKIZI.

Na, Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Jamii ya Wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini Unguja, imetakiwa kuchukua tahadhari za haraka kufuatia kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria, hali inayozua wasiwasi miongoni mwa wakazi na wadau wa afya katika eneo hilo.

Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Uhamasishaji cha Programu ya Kutokomeza Malaria Zanzibar, imeendesha kikao na wadau mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na kutathmini hali ya ugonjwa huo.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Kituo cha Walimu Mkwajuni, Afisa Uhamasishaji wa Programu hiyo kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Salum Faki Salum, amesema hali ya maambukizi ya malaria ni tete katika wilaya hiyo, hususan katika shehia za Nungwi ambazo zimeonekana kuwa na idadi kubwa ya waathirika. Amesema katika kipindi cha wiki iliyopita, jumla ya kesi 46 zimeripotiwa, ambapo kesi 43 ni za ndani na kesi 3 zimetokea nje ya eneo hilo.

Amebainisha kuwa makundi yaliyoathirika zaidi ni wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45, wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara wadogo kama mama lishe na wauza madukani, wafanyakazi wa ujenzi pamoja na walinzi wa mahoteli sambamba na sehemu za mikusanyiko ya watu wenye kufuata wifi za bure katika mahotel.

Aidha, Salum amesema Wizara ya Afya imechukua hatua stahiki za kukabiliana na ongezeko hilo la maambukizi, ikiwemo kuimarisha kampeni za uhamasishaji kwa jamii  na kuongeza ufuatiliaji na udhibiti wa mazalia ya mbu katika maeneo hatarishi. Ameeleza kuwa juhudi hizo zinaendelea sambamba na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa kwa ufanisi.

Salum amesema ongezeko hilo linachangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo uchafu wa mazingira na kutotumia njia sahihi za kujikinga na maradhi hayo, hasa katika msimu wa mvua unaosababisha mazalia ya mbu aina ya Anopheles, wanaosambaza vimelea vya malaria.

Hivyo, ameihimiza jamii kuchukua hatua za kinga ikiwemo kudumisha usafi wa mazingira, kuondoa maji yaliyotuama na kutumia vyandarua vyenye viuatilifu.

Kwa upande wake, Afisa Afya wa Kitengo cha Elimu Wilaya ya Kaskazini A, Afife Ali Mussa, amesema ni muhimu kwa wananchi kushirikiana na wataalamu wa afya ili kudhibiti ugonjwa huo, hasa katika maeneo yenye muingiliano mkubwa wa watu kama Nungwi.

Aidha, amewahimiza wananchi kufika katika vituo vya afya mara wanapoanza kuhisi dalili za malaria zikiwemo homa, maumivu ya kichwa na uchovu wa mwili, ili kupata uchunguzi na matibabu mapema.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha afya ya jamii na kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuboresha sekta ya afya.

Wakati huo huo, washiriki wa kikao hicho wameeleza kuwa uwepo wa bandari zisizo rasmi pamoja na uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya biashara na ujenzi ni miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa maambukizi ya malaria.

Washiriki hao wameahidi kushirikiana na mamlaka husika na kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii ili kuhakikisha ugonjwa wa malaria unatokomezwa katika Wilaya ya Kaskazini A.