Popular services

MHE. AYOUB NA USONGE WASHIRIKI IFTAR ILIYOANDALIWA NA UVCCM; VIJANA WAHIMIZWA KUTENDA MEMA

 MHE. AYOUB NA USONGE WASHIRIKI IFTAR ILIYOANDALIWA NA UVCCM; VIJANA WAHIMIZWA KUTENDA MEMA

Na Nishan Khamis, Chaani
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kaskazini A umeandaa futari maalum iliyowakutanisha vijana wa chama, mayatima pamoja na wananchi kwa ujumla katika Tawi la CCM Chaani Masingini.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, viongozi na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kaskazini A, Ramadhan Masoud Machano, amesema futari hiyo ni sehemu ya juhudi za umoja huo kuimarisha mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ameeleza kuwa UVCCM imeona umuhimu wa kuwashirikisha vijana na mayatima katika hafla hiyo ili kuwapa faraja na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya jamii, huku akisisitiza kuwa umoja huo utaendelea kuandaa shughuli za kijamii zinazolenga kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji.

Aidha, amewashukuru viongozi, wadau na wananchi waliojitokeza kushiriki futari hiyo, akisema ushiriki wao unaonesha mshikamano mkubwa uliopo katika jamii na ndani ya chama.

Mgeni rasmi katika futari hiyo alikuwa Mbunge wa Jimbo la Chaani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Ayoub amewahimiza vijana kuendelea kutenda mema na kujiepusha na mambo mabaya, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Eid al-Fitr.

Aidha, amewataka viongozi wa UVCCM Wilaya ya Kaskazini A kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele pindi fursa mbalimbali zinapojitokeza, bila kujali vyama vyao vya kisiasa, kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Juma Usongwe Hamad, amepongeza uongozi wa UVCCM kwa kuandaa futari hiyo iliyowakutanisha vijana, mayatima na wananchi kwa ujumla bila kujali itikadi za kisiasa.

Amesema shughuli kama hizo zinaimarisha mshikamano wa kijamii na kuonesha umuhimu wa kushirikiana katika kusaidia makundi yenye uhitaji ndani ya jamii.