Popular services

DKT. MAHMOUD ATAMANI KUIFANYA TUMBATU KUWA KITUO BORA CHA KUHIFADHI QUR’AN NCHINI.

 DKT. MAHMOUD ATAMANI KUIFANYA TUMBATU KUWA KITUO BORA CHA KUHIFADHI QUR’AN NCHINI

Na: Nishan Khamis
Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Mhe. Dkt. Mahmoud Omar Hamad, amesema kuwa katika kuhakikisha kisiwa hicho kinakuwa kituo bora cha kuhifadhi Qur’an Tukufu (Tahfidh), ni wajibu kwa wazazi, walezi na walimu wa madrasa kushirikiana katika usimamizi wa kitaaluma kwa wanafunzi wa madrasa.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha kisiwa hicho kinakuwa mstari wa mbele katika kuzalisha wasomi bora wa Tahfidh Qur’an nchini.

Dkt. Mahmoud ameyasema hayo leo alipokuwa mgeni rasmi katika mashindano ya Tahfidh Qur’an Tukufu yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Walimu wa Madrasa Kisiwa cha Tumbatu, Wilaya Ndogo ya Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema ni muhimu kuandaa mikakati madhubuti ya kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema na kuwajengea msingi imara wa elimu ya dini pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla, ili kuepukana na vishawishi vya ulimwengu na kuifanya Tumbatu kuwa mfano bora wa wasomi wa Tahfidh Qur’an nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Juma Othman Hija, amesema kutokana na changamoto za utandawazi wa sasa, ni vyema wazazi, walezi, walimu wa madrasa pamoja na viongozi kwa ujumla kushirikiana kwa karibu katika kuwalea watoto kimaadili na kuwahimiza kupata elimu zote kwa manufaa ya maisha ya duniani na Akhera.

Awali akisoma risala katika hafla hiyo, Ostaz Juma Gora Khamis amesema jumuiya hiyo ina miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, na lengo kuu ni kuwaunganisha walimu wa madrasa pamoja na jamii ili kuendeleza maendeleo ya elimu katika kisiwa hicho.

Amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo ni ukosefu wa ofisi, vifaa vya kufundishia, pamoja na ukosefu wa uwezeshaji kwa walimu ili waweze kujikimu kimaisha.

Ameongeza kuwa jumla ya wanafunzi 28 wameshiriki mashindano hayo, ambapo wanafunzi wa kiume walikuwa 8 na wa kike 20. Washindi pamoja na washiriki wote walipatiwa fedha taslimu kama zawadi ya kuwapongeza kwa juhudi zao.