Popular services

DIWANI DACHI NA VIONGOZI WENZAKE WATOA SADAKA YA MCHELE KWA ZAIDI YA KAYA 700, MHE. AYOUB ATOA SALAMU

 

Na Nishan Khamis, Gamba
Zaidi ya kaya 700 za watu wenye mahitaji maalum katika Wilaya ya Kaskazini A zimepatiwa sadaka ya mchele kilo 25 kwa kila kaya, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Chaani, Bi  Rukia Jabir Khamis amesema kuwa msingi wa maendeleo ni umoja na mshikamano katika jamii, jambo ambalo husaidia kuleta mafanikio ya kimaendeleo.

Amesema kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya Kaskazini A na mkoa kwa ujumla kuendelea kudumisha amani na utulivu, kwani ndiyo nguzo muhimu ya kuendeleza maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kuteuliwa Wilaya ya Kaskazini A, Ali Chumu Haji (Dachi) amesema kuwa kwa kushirikiana na viongozi wenzake wamefanikiwa kutoa sadaka hiyo kwa watu wenye mahitaji maalum wilayani humo ili kuwasaidia katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesema sadaka hiyo imelenga makundi hayo kutokana na changamoto za maisha wanazokabiliana nazo, huku akiahidi kuwa viongozi hao wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi hao wanapata msaada hasa wa chakula cha iftar na daku katika kipindi cha Ramadhani.

Aidha, amewahimiza watu wenye uwezo kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hususan katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ili kupata fadhila mbele ya Mwenyezi Mungu. Amesema zaidi ya shilingi milioni 22 zimetumika kununua chakula hicho.

Baadhi ya wananchi waliopokea sadaka hiyo wameushukuru uongozi kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia, huku wakiomba utamaduni huo wa kutoa sadaka uendelezwe kwa maslahi mapana ya maendeleo ya jamii katika wilaya hiyo.