Na,Nishan khamis, Chaani.
Viongozi wa Jimbo la Chaani, Mheshimiwa Mbunge Ayoub Mohammed Mahmoud na Mwakilishi Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, wametenga kiasi cha shilingi milioni 57 kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili wavuvi na wakulima wa mwani katika jimbo hilo.
Hatua hiyo imetangazwa jana na Mwakilishi huyo wakati akizungumza katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, ambapo kilihudhuriwa na Kamati za Maendeleo ya Jimbo pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Juma Usonge Hamad alisema kuwa fedha hizo zinalenga kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wanaojihusisha na sekta za uvuvi na kilimo cha mwani, ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi wa eneo hilo, alisisitiza kuwa ni muhimu kuweka mazingira bora ya uzalishaji ili kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo endelevu.
Amesema ni wajibu kuhakikisha wananchi wetu wanapata msaada unaohitajika ili kuinua maisha yao. Uwekezaji huu ni sehemu ya dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto zao kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Mbunge Ayoub Mohammed Mahmoud alishiriki kikao hicho kwa njia ya mtandao, ambapo alieleza kuunga mkono jitihada hizo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kufanikisha miradi ya maendeleo.
Amesema maendeleo ya jimbo letu yanategemea mshikamano wetu. Ni lazima tushirikiane kuhakikisha rasilimali hizi zinatumika kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi wote.
Naye Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Adam Abdalla Makame, aliwapongeza viongozi hao kwa hatua yao ya kuwajali wananchi na kuchukua maamuzi yenye tija kuwa uwekezaji huo ni mfano mzuri wa uongozi unaojali maendeleo.
Wajumbe wa kikao hicho kwa pamoja walipongeza na kuunga mkono juhudi za viongozi wao, wakieleza kuwa hatua hiyo italeta matumaini mapya kwa wananchi wa Jimbo la Chaani. Walisisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu kati ya serikali, viongozi na jamii ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa mafanikio.

