Popular services

DKT. MAHMOUD APOKELEWA KWA SHANGWE TUMBATU KATIKA TAMASHA LA WAVUVI

 DKT. MAHMOUD APOKELEWA KWA SHANGWE TUMBATU KATIKA TAMASHA LA WAVUVI

MWANDISHI: NISHAN KHAMIS, TUMBATU
Jamii ya Kisiwa cha Tumbatu imetakiwa kuendelea kuthamini na kuilinda sekta ya uvuvi, ikielezwa kuwa ni nguzo muhimu ya ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.

Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Dkt. Mahmoud Omar Hamad, alipokuwa akizungumza kama mgeni rasmi katika Tamasha la Wavuvi lililofanyika leo kisiwani humo.

Amesema sekta ya uvuvi inachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa pamoja na kutoa ajira za kujiajiri kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa wavuvi kufuata sheria na taratibu za uvuvi pamoja na kulinda rasilimali za bahari ili ziweze kudumu kwa vizazi vijavyo.

Aidha, Dkt. Mahmoud amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika jamii, akiahidi kuendelea kushirikiana na wakazi wa jimbo hilo katika kuendeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. Katika kuunga mkono juhudi hizo, amechangia shilingi milioni moja kwa ajili ya tamasha hilo.

Awali, akisoma risala katika tamasha hilo, Mwenyekiti Abdul Kombo Ali amesema kuwa tamasha hilo sasa linaingia mwaka wa nne tangu kuanzishwa kwake, likiwa na lengo la kuimarisha umoja wa wavuvi pamoja na jamii kwa ujumla ili kukuza maendeleo ya Kisiwa cha Tumbatu.

Hata hivyo, ameainisha changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uvuvi kuwa bado inawakabili wavuvi wengi wa eneo hilo, hali inayodhoofisha juhudi zao za kiuchumi.

Tamasha hilo limepambwa na michezo mbalimbali ya asili na ya kisasa, maonesho ya shughuli za baharini pamoja na utoaji wa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira ya bahari, kwa lengo la kuhakikisha maendeleo endelevu.