Na Nishan Khamis, Chaani
Walimu na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Mapinduzi iliyopo Chaani wamesema ukosefu wa vyumba vya madarasa vya kutosha, uzio wa skuli pamoja na upungufu wa walimu ni changamoto zinazowaletea usumbufu mkubwa katika shughuli za ufundishaji.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa Jimbo la Chaani ya kukabidhi fedha kwa ajili ya posho za walimu wanaojitolea kufundisha katika skuli hiyo, Mwalimu Mkuu Msaidizi Bakar Ali Makame amesema licha ya jitihada zinazofanywa na viongozi wa jimbo hilo katika kuimarisha sekta ya elimu, bado kuna changamoto kadhaa zinazoikabili skuli hiyo.
Ameeleza kuwa upungufu wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa uzio wa skuli pamoja na uhaba wa walimu vinaathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya ufundishaji.
Akikabidhi fedha hizo kwa niaba ya viongozi wa jimbo, Diwani wa Wadi ya Chaani Khamis Haji Khamis amesema kuwa viongozi wa jimbo hilo wamekusudia kuleta mageuzi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu.
Ameongeza kuwa fedha hizo zimetolewa kwa ushirikiano wa viongozi wa jimbo hilo kwa ajili ya kuwasaidia walimu wanaojitolea katika skuli hiyo ili kuwapa motisha katika majukumu yao ya kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora.
Aidha, amewahakikishia walimu na uongozi wa skuli hiyo kuwa viongozi wa jimbo hilo wataendelea kushirikiana nao katika kuimarisha maendeleo ya elimu katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli hiyo Othman Omar amewapongeza viongozi wa jimbo kwa hatua hiyo, sambamba na kuiomba Wizara ya Elimu kuongeza idadi ya walimu katika skuli hiyo ili kuboresha zaidi mazingira ya ufundishaji.
