Popular services

DIWANI MAIMUNA KASSIM AKABIDHI MISAHAFU NA JUZUU MADRASAT ISTIQAMA KIVUNGE, AHIMIZA MALEZI YA MAADILI KWA WATOTO.

 

NISHAN KHAMIS, KIVUNGE
Diwani wa Viti Maalum Wilaya ya Kaskazini A, Maimuna Kassim Yussuf, amewataka walimu wa madrasa pamoja na wazazi kushirikiana katika kuwalea watoto katika maadili mema sambamba na kuwapa elimu ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji.

Diwani Maimuna ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi katika mashindano ya kuhifadhi Qur’an yaliyofanyika katika Madrasat Istiqama Kivunge, Wilaya ya Kaskazini A.

Amesema ushirikiano kati ya walimu na wazazi ni muhimu katika kuwalea watoto kimaadili jambo ambalo litawasaidia kuwaepusha na vitendo vya udhalilishaji. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani na utulivu akieleza kuwa hali hiyo ni msingi muhimu katika kuendeleza maendeleo ya nchi.

Halikadhalika,  amewahakikishia kuchukua changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi. Katika hafla hiyo alikabidhi misahafu na juzuu ili kusaidia wanafunzi wa madrasa hiyo huku akiwapongeza walimu wanawake kwa juhudi zao katika kuhakikisha maendeleo bora ya wanafunzi.

Akitoa neno la shukrani, Mwalimu Mkuu wa Madrasat Istiqama, Tatu Khamis Issa, alimpongeza Diwani huyo kwa ushirikiano wake na kueleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa vikalia, misahafu, juzuu, uhaba wa majengo pamoja na feni katika madrasa hiyo.
Amesema madrasa hiyo ina jumla ya wanafunzi 150 huku mashindano hayo yakihusisha uhifadhi wa Qur’an kuanzia juzuu ya kwanza hadi ya ishirini.

Naye mzazi Amina Haji Haji ametoa wito kwa viongozi wa jimbo hilo pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia kutatua changamoto za madrasa hiyo kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya elimu kwa vijana nchini.