Na, Nishan Khamis, Zanzibar
Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ limesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imedhamiria kuwainua kiuchumi wanawake wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapatia mikopo mbalimbali itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika ziara maalum ya kutembelea miradi sambamba na kuwahamasisha wanawake kuzikimbilia fursa za mikopo itakayowainua kiuchumi, Afisa Wajasiriamali wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Foum Haji Khatib, amesema serikali imeandaa mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapatia mikopo itakayowasaidia kukuza biashara zao kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Ametoa wito kwa wajasiriamali hao kufuata utaratibu unaotakiwa ili waweze kupata mikopo hiyo kwa urahisi zaidi, sambamba na kuwa na miradi bora itakayowasaidia kuinuka kiuchumi.
Amesema Baraza la Manispaa litaendelea kushirikiana nao ili kuwasaidia kufikia malengo yao ya kiuchumi kwa maslahi mapana ya wilaya na taifa kwa ujumla. Amesema zaidi ya vikundi vinne vilitembelewa katika wilaya hiyo kwa lengo la kuongeza hamasa kwa wanawake wajasiriamali kuzikimbilia fursa za mikopo nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajasiriamali hao wametoa pongezi kwa ziara hiyo wakisema ni hatua nzuri kwa viongozi kuona umuhimu wa kuinuka kiuchumi kwa wanawake. Hata hivyo, wametoa wito wa kupunguziwa masharti ya mikopo ili iweze kupatikana kwa urahisi na kwa wakati muafaka, jambo litakalosaidia kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo yao pamoja na taifa kwa ujumla.

