Popular services

ALIYEZAMA KATIKA BWAWA LA CHAANI MASINGINI APATIKANA AMEFARIKI.

 ALIYEZAMA KATIKA BWAWA LA CHAANI MASINGINI APATIKANA AMEFARIKI

Na: Nishan Khamis, Chaani
Mashauri Abdalla Mashauri, mkazi wa Shehia ya Mwakaje, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 39 hadi 40, aliyeripotiwa kuzama jana majira ya saa sita na dakika 40 mchana katika bwawa la Chaani Masingini, amepatikana leo majira ya saa tatu na robo asubuhi akiwa amefariki.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Mkuu wa Waokozi wa Baharini kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, Mohammed Idarus Mohammed, amesema walipokea taarifa za tukio hilo jana majira ya saa saba mchana na kufika katika eneo hilo kuanza jitihada za uokozi.

Amesema licha ya juhudi hizo, hawakufanikiwa kuupata mwili huo jana kutokana na changamoto ya maji mengi pamoja na tope lililokuwemo katika bwawa hilo. Hata hivyo, leo majira ya saa tatu na robo asubuhi waliweza kuupata mwili huo ukiwa tayari umefariki.

Aidha, ametoa wito kwa jamii kutoa taarifa haraka kwa vikosi vya uokozi pindi majanga kama hayo yanapotokea ili hatua za uokozi ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Chaani Masingini, Mustafa Ahmada Ali, amesema alipata taarifa ya tukio hilo jana majira ya saa sita mchana na kufika katika eneo la tukio, kisha kutoa taarifa kwa kikosi cha uokozi ambacho kilifika na kuanza jitihada za kumtafuta mtu huyo.
Ameeleza kuwa pamoja na jitihada hizo, hawakuweza kuupata mwili huo jana kutokana na changamoto ya maji mengi na tope katika bwawa hilo.

Sheha huyo ameongeza kuwa hii ni mara ya pili kutokea kwa kifo katika bwawa hilo, hivyo ametoa wito kwa jamii kuwa makini zaidi pamoja na kuchukua hatua za haraka wanapokutana na majanga kama hayo.

Naye Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Ali, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa jimbo hilo, amewataka wakaazi wa Chaani, hasa wazazi, kuwa makini na watoto wao wanapokuwa karibu na bwawa hilo. Pia ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu kwa msiba huo.

Kwa upande wake, Simai Ali Pandu, mkazi wa Mfenesini kwa Daruweshi na mmoja wa wavuvi wanane waliokuwa wakivua samaki katika bwawa hilo, amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa sita mchana wakati wakiendelea na shughuli zao za uvuvi.

Amesema mwenzake huyo alizidiwa na maji wakati wakiwa katika shughuli hiyo, na kuongeza kuwa ni kawaida kwao kuvua samaki katika bwawa hilo, lakini kwa bahati mbaya tukio hilo lilitokea kwa mwenzao siku ya jana.