Popular services

 Na,Nishan khamis, Chaani.

Uongozi wa Jimbo la Chaani umefanya ziara ya kuwatembelea na kuwafariji wananchi walioathirika na maafa ya mvua kubwa zilizonyesha juzi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na kusababisha uharibifu wa baadhi ya nyumba pamoja na mali za wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo , Diwani wa Wadi ya Chaani Khamis Haji Ali alisema uongozi wa jimbo umefika kuwafariji wananchi waliopatwa na maafa hayo na kuwahakikishia kuwa viongozi wanaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuona namna bora ya kuwasaidia walioathirika.

Alisema mvua hizo zimesababisha madhara katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo ikiwemo kuharibika kwa nyumba na mali za wananchi, huku akiwataka wananchi kuwa na subira wakati juhudi za kuwasaidia zinaendelea kufanywa na viongozi pamoja na taasisi mbalimbali.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum  Maimuna Kassim Yussuf aliwataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi katika kipindi hiki cha mvua kwa kuhakikisha wanakaa katika maeneo salama na kuchukua hatua za haraka pindi wanapoona dalili za hatari zinazoweza kusababisha madhara.

Naye Diwani wa Kuteuliwa wa Jimbo  Subira Ali Juma alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na mvua kubwa, huku akiwataka wananchi kuendelea kufuata ushauri na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika ili kuepusha madhara zaidi.

Kwa upande wao, wananchi walioathirika na maafa hayo waliushukuru uongozi wa jimbo kwa kuwafikia na kuwafariji katika kipindi kigumu wanachokipitia. Walisema ujio wa viongozi hao umewapa faraja na matumaini, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi katika juhudi za kurejesha hali ya maisha yao kuwa ya kawaida.