Popular services

VIONGOZI WA JIMBO LA CHAANI WAONESHA DHAMIRA YA CHAANI MPYA, ZAIDI YA WATU 1,000 WASHIRIKI IFTAR.

 

Na Nishan Khamis, Chaani.
Mbunge wa Jimbo la Chaani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema ameridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika mashindano ya Qur’an pamoja na iftar ya pamoja iliyofanyika katika jimbo hilo.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mhe. Ayoub Mohammed amesema kuhifadhi Qur’an ni jambo lenye historia kubwa na umuhimu kwa waumini wa dini ya Kiislamu, hivyo mashindano hayo yana mchango mkubwa katika kuwajenga vijana na jamii kwa ujumla katika misingi ya maadili mema.
Amesema ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwalea watoto katika mafunzo ya Qur’an ili kuwajengea maadili bora na kuwasaidia kuepukana na mienendo mibaya katika jamii.

Aidha, amepongeza wananchi wa Jimbo la Chaani kwa ushirikiano wao pamoja na maandalizi mazuri ya hafla hiyo, akisisitiza kuwa viongozi wa jimbo hilo wamejipanga kuendeleza mashindano hayo ili yawe makubwa zaidi na yenye ubora wa kipekee, jambo litakalolipa heshima jimbo hilo pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano wa wananchi bila kujali itikadi za kisiasa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Mhe. Juma Usonge Hamad, amesema kuwa mashindano hayo yamehusisha zaidi ya madrasa 60 kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo huku jumla ya washiriki 241 wakiwemo wanafunzi na watu wazima wakishiriki katika kusoma na kuhifadhi Qur’an Tukufu kuanzia Juzuu moja hadi ishirini.

Amesema mwitikio huo mkubwa unaonesha namna wananchi wa Chaani wanavyothamini mafunzo ya dini na juhudi za kuwajenga vijana katika misingi ya maadili mema.

Zaidi ya watu 1,000 walijitokeza kushiriki iftar ya pamoja iliyoandaliwa na viongozi wa Jimbo la Chaani pamoja na familia ya Mheshimiwa mbunge wa jimbo hilo.
Katika mashindano hayo, jumla ya washindi 38 walipatikana ambapo washindi waliopata nafasi kuanzia juzuu ya kwanza hadi ya 20 walizawadiwa misahafu pamoja na fedha taslimu.
Kwa upande wao, washiriki wa mashindano hayo pamoja na wageni waliohudhuria iftar hiyo wamewapongeza viongozi wa Jimbo la Chaani kwa juhudi zao za kuimarisha umoja na ushirikiano, wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano huo kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo na Zanzibar kwa ujumla.