Na Nishan Khamis – Mkwajuni
Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, Khamis Ali Vuai, amewahakikishia walimu na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Mkwajuni kuwa viongozi wa jimbo hilo wataendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuwalea wanafunzi katika maadili mema sambamba na kuongeza ufaulu mzuri wa kitaaluma kwa maendeleo bora ya elimu katika jimbo hilo.
Mhe. Mbunge ameyasema hayo leo katika mashindano ya Tahfidh Qur’an yaliyofanyika Skuli ya Sekondari Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, yaliyoandaliwa na Kamati ya Da’awa ya skuli hiyo, ikiwa ni miaka sita tangu kuanzishwa kwake.
Katika hafla hiyo, Mbunge aliambatana na madiwani wote wa jimbo hilo pamoja na Kamati ya Siasa ya Jimbo la Mkwajuni, akionyesha mshikamano wa viongozi katika kuendeleza elimu na maadili kwa wanafunzi.
Amesema kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake jimbo hilo wamefurahishwa na tukio hilo na kuahidi kushirikiana kikamilifu katika harakati hizo, akiwahakikishia kushughulikia changamoto za ujenzi wa msikiti uliopo katika eneo la skuli pamoja na changamoto zingine kwa mustakabali mzuri wa maendeleo ya skuli hiyo.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Mustafa Makame Hamad, amesema lengo kuu la kuanzishwa mashindano hayo ni kuwajenga wanafunzi kuwa na maadili mema na kukuza vipaji vyao vya kielimu kwa mustakabali mzuri wa maisha yao.
Awali, mwanafunzi Khairat Zaidu alisema miongoni mwa changamoto zao katika kamati yao ni ukosefu wa kompyuta, ofisi rasmi pamoja na upungufu wa fedha kwa ajili ya maandalizi ya mashindano na zawadi kwa washindi.
Mashindano hayo yalihusisha wanafunzi wa skuli hiyo katika Tahfidh Qur’an Juzuu 3, 5, 7, 10 na 15, sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi. Aidha, watoto yatima na wanafunzi wenye mazingira magumu walipewa sadaka ya iftar katika hafla hiyo, kama ishara ya umoja na ushirikiano katika skuli hiyo.

