DKT. MAHMOUD ATOA WITO KUIMARISHWA USOMAJI WA QUR’AN KWA WATOTO TUMBATU
NISHAN KHAMIS, ZANZIBAR.
Wazazi na walimu wa madrasa katika Jimbo la Tumbatu wametakiwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha watoto wanajifunza na kuhifadhi Qur’an Tukufu ili kuwajengea misingi imara ya maisha ya hapa duniani na kesho Akhera.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Mheshimiwa Dkt. Mahmoud Omar Hamad, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Qur’an yaliyofanyika katika Shehia ya Pale, ambapo amesisitiza kuwa kila familia ina wajibu wa kusimamia malezi ya dini kwa watoto.
Amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja, hususan Kisiwa cha Tumbatu, una historia kubwa ya kutoa wanazuoni na mashekhe, hivyo ni muhimu kuendeleza jitihada hizo kwa ushirikiano kati ya wazazi na walimu.
Aidha, amewahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanasoma na kuhifadhi Qur’an kwa ufasaha ili kujenga maadili mema na mustakabali bora wa maisha yao.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Makame, Moss Makame, amewataka wananchi kushirikiana na Mwakilishi wa Jimbo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa kwa maendeleo ya jamii.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo sheha wa heshia ya pel Makame Mossi Makame ametoa pongezi za dhati kwa mgeni rasmi na kufarajika kuona juhudi zake mgeni ,sambamba na hayo kuwaomba wakuu simi kumuunga mkono katika kuleta maendeleo ya jimbo hilo.
Mashindano hayo yamehusisha takriban vyuo saba kutoka Jimbo la Tumbatu, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, yakihusisha kuhifadhi Qur’an Tukufu kuanzia Juzuu ya kwanza hadi ya 30.
