Popular services

 Na,Nishan khamis, MKOKOTONI.

Diwani wa Wadi ya Kipange, Jimbo la Tumbatu, Khamis Kombo Khamis amewasisitiza walimu na wanafunzi kuendelea kushirikiana katika kuendeleza maendeleo ya elimu katika wadi hiyo, sambamba na kuongeza juhudi katika kujifunza na kuhifadhi Qur’an Tukufu ili kuwajengea wanafunzi maadili mema.

Diwani Khamis ameyasema hayo leo alipokuwa mgeni rasmi katika mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Mkokotoni, yaliyoandaliwa na Kamati ya Daawa ya wanafunzi wa shule hiyo.

Aidha, amewahakikishia wanafunzi na walimu kuwa ataendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo. Amesema katika awamu ijayo mashindano hayo yataandaliwa kwa ubora zaidi ili kuhamasisha vijana wengi kujitokeza kushiriki katika kuhifadhi Qur’an Tukufu, jambo ambalo ni muhimu kwa maisha ya hapa duniani na Akhera.

Pia amewataka wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao pamoja na kuwa mstari wa mbele kuhubiri amani na utulivu nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mwalimu Mkuu wa Sekondari Mkokotoni, Asha Said Ali, ametoa pongezi kwa ushirikiano mkubwa uliooneshwa na wanafunzi pamoja na walimu katika kufanikisha mashindano hayo. 
Amesema ushirikiano huo ni chachu ya kuendeleza maendeleo ya shule hiyo, hivyo amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano katika kuendeleza elimu.

Awali, mwanafunzi Mulhat Juma Haji akisoma risala katika hafla hiyo alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia kamati hiyo katika kuandaa mashindano na kuibua vipaji vya wanafunzi, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vitabu vya dini, mtazamo potofu wa baadhi ya wanafunzi kuhusu kamati hiyo pamoja na kukosa ushirikiano mzuri kutoka kwa baadhi ya walimu.

Mashindano hayo yalihusisha kuhifadhi juzuu ya kwanza, ya pili na ya tatu za Qur’an Tukufu, yakishirikisha wanafunzi kutoka shule za Msingi na Sekondari Mkokotoni. Washindi pamoja na washiriki wote walipatiwa zawadi za misahafu na fedha taslimu.