Na Nishan Khamis, Chaani
Zaidi ya watu 2,000 wakiwemo wenye mahitaji maalum kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja leo wamepatiwa sadaka ya iftar iliyoandaliwa na viongozi wa Jimbo la Chaani katika kiwanja cha mpira cha Sulubu, Pwani Mchangani, Wilaya ya Kaskazini A.Katika hafla hiyo, wananchi waliopatiwa sadaka hiyo walikabidhiwa msaada wa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, sukari, tende, unga wa ngano pamoja na mafuta ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema viongozi wa jimbo hilo wamejipanga kuwatumikia wananchi kwa vitendo kwa kuleta maendeleo kama walivyoahidi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi.
Amesema utoaji wa sadaka hiyo ya iftar ni sehemu ya kuonyesha mshikamano na kuwafariji wananchi, akibainisha kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa mipango mingi ya maendeleo inayolenga kuimarisha ustawi wa wananchi wa jimbo hilo.
Aidha amesema viongozi wa jimbo hilo wamekusudia kufanya shughuli kama hiyo kuwa utamaduni wa kudumu, huku wakitafuta ushirikiano wa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kufanikisha azma ya kujenga Chaani Mpya ya Mabadiliko kwa Wote.
Pia amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, ushirikiano na amani miongoni mwa wananchi, akiwataka kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga mshikamano wa jamii.
Sambamba na hilo, amewahimiza wananchi kuendelea kuwaunga mkono viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zao za kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Mhe. Juma Usonge Hamad, amesema zaidi ya watu 2,000 wamefikiwa na sadaka hiyo ya iftar na kwamba mpango huo utaendelea katika kipindi chote cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hadi kufikia Sikukuu ya Idd el-Fitr.
Amesema dhamira ya viongozi wa jimbo hilo ni kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinaguswa na mpango huo, huku wakilenga kufanya Jimbo la Chaani kuwa mfano wa maendeleo kwa majimbo mengine.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo wamesema hatua hiyo ni mwanzo mzuri ulioanzishwa na viongozi wao, wakieleza kuwa inaonyesha kujali ustawi wa wananchi na wameahidi kuendelea kuwaunga mkono katika juhudi za kuleta maendeleo katika jimbo hilo.


