Na Nishan Khamis, Kaskazini Unguja
Mwenyekiti wa Chipukizi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Aymar Omar Mohammed, amefanya ziara maalum na kukutana na wajumbe wa Kamati Tendaji wa Chipukizi kuanzia ngazi ya majimbo, wilaya na mkoa kwa lengo la kuwafariji kamati za uendeshaji za Chipukizi ndani ya mkoa huo pamoja na kukagua mradi wa kitega uchumi wa Chipukizi uliopo Pangeni, Wilaya ya Kaskazini B.
Akizungumza katika ziara hiyo, Aymar amesema kuwa mradi huo wa kitega uchumi utasaidia kwa kiasi kikubwa wanachama wa Chipukizi kujikwamua kiuchumi mara baada ya kukamilika kwake. Amesisitiza kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wanachama wa jumuiya hiyo pamoja na kuimarisha shughuli za maendeleo ndani ya Chipukizi na CCM kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu wa Uhamasishaji wa Chipukizi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Suleiman Gulam Juma, ametoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Chipukizi wa mkoa huo kwa kuandaa kikao na wajumbe pamoja na kufanya ziara ya kukagua mradi huo wa ujenzi wa milango ya maduka.
Amesema kuwa hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 75, na kutoa shukrani kwa wadau mbalimbali waliochangia katika kufanikisha hatua hiyo ya ujenzi. Aidha, ametoa wito kwa wanachama na wadau kuendelea kushirikiana ili kukamilisha mradi huo kwa manufaa ya maendeleo ya Chipukizi na CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika ziara hiyo pia wamempongeza kiongozi wao kwa juhudi anazozifanya katika kuendeleza jumuiya hiyo na kumuahidi kuendelea kumuunga mkono katika kuimarisha na kuendeleza shughuli za maendeleo ya Chipukizi. Halima Rajab kamau.


