MHE,AYOUB, USONGE NA EAF WAENDELEA KUSAMBAZA NEEMA YA SADAKA JIMBO LA CHAANI
Na Nishan Khamis, ChaaniKatibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, ametoa wito kwa wadau na viongozi mbalimbali kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu, hasa katika kustawisha maendeleo ya maisha yao.
Katibu Debe amesema hayo leo katika Jimbo la Chaani wakati wa hafla ya utoaji wa sadaka ya Iftar iliyoandaliwa na taasisi ya Noor Yaqeen Foundation kwa kushirikiana na European Aid Foundation (EAF) pamoja na viongozi wa Jimbo la Chaani. Katika hafla hiyo, jumla ya kaya mia sita zilipatiwa sadaka hiyo, zikiwemo kaya mia moja za watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya viongozi wenzake, alitoa shukrani kwa European Aid Foundation (EAF) kwa ushirikiano wao katika kusaidia wananchi wa jimbo hilo.
Aidha, aliwasisitiza wananchi wa Jimbo la Chaani kuwa dhamira ya Chaani Mpya, Maendeleo kwa Wote yanaendelea kutekelezwa kwa vitendo,hivyo akawanasihi kuendelea kushirikiana katika kuleta maendeleo ya jimbo hilo.
Naye Mweka Hazina wa taasisi ya Noor Yaqeen, Kassim Abdalla Abeid, amesema jumla ya kaya mia sita zimepatiwa sadaka hiyo, wakiwemo watu wenye ulemavu mia moja, wajane, mayatima, wazee pamoja na watu wanaoishi katika mazingira magumu. Alifafanua kuwa walipatiwa msaada wa vyakula ikiwemo unga wa ngano, sukari, mchele, mafuta na chumvi.
