Na,Nishan khamis, Kivunge.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Atai Masoud, amewapongeza wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge kwa uwajibikaji wao na juhudi wanazozifanya katika kutoa huduma kwa wananchi.Akizungumza wakati wa hafla ya iftar iliyoandaliwa na hospitali hiyo, amesema anatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi wa sekta ya afya na kuahidi kushughulikia baadhi ya changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma.
Aidha, ameahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa hafla ya iftar ya mwaka ujao inakuwa kubwa zaidi na yenye manufaa makubwa kwa jamii.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Baraza la manispaa wilaya ya kaskazini A Nyange Kheri Ali ameipongeza kamati iliyoandaa hafla hiyo kwa maandalizi mazuri yaliyowezesha kukusanyika kwa pamoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kuahidi kuendelea kushirikiana na kamati hiyo pamoja na madiwani wenzake katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Naye Ali Omar Ali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Kivunge Saifee, amepongeza umoja na mshikamano uliopo baina ya viongozi, wananchi na hospitali hiyo, akisema ushirikiano huo unasaidia kuimarisha utoaji wa huduma na kuleta maendeleo katika sekta ya afya kwa jamii inayozunguka hospitali hiyo.
