Popular services

ZAIDI YA KAYA 100 WADI YA GAMBA ZAPATIWA SADAKA YA IFTAR KUTOKA LEGACY AID GROUP.

 

Na, Nishan Khamis – Gamba
Zaidi ya kaya 100 katika wadi ya Gamba, wilaya ya Kaskazini A, zimepatiwa sadaka ya iftar kutoka taasisi ya Legacy Aid Group kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaoishi katika mazingira magumu wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa sadaka iliyofanyika katika kijiji cha Matemwe Mbuyuni na Gamba, Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Gamba, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, amewashauri wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum pamoja na wale wanaoishi katika hali ngumu, hasa katika kipindi hiki cha Ramadhani, ili waweze kufunga na kumaliza mfungo wao katika hali bora ya upatikanaji wa iftar na daku.

Mheshimiwa Nyange amesema mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kipindi muhimu cha kuonyesha mshikamano na huruma kwa jamii. Ameipongeza taasisi ya Legacy Aid Group kwa kuona umuhimu wa kutoa msaada huo kwa wananchi wa Wadi ya Gamba, akieleza kuwa wengi wao ni wa kipato cha chini na msaada huo umewafikia walengwa stahiki kulingana na hali zao.

Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia wananchi hao, si tu katika kipindi cha Ramadhani bali pia kuelekea Sikukuu na nyakati nyingine, ili kuchangia maendeleo ya wadi hiyo.

Kwa upande wake, Mhasibu wa taasisi ya Legacy Aid Group, Faudhia Ahmed Hassan, amesema utoaji wa sadaka hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa taasisi hiyo katika kusaidia jamii kwenye nyanja mbalimbali. Amehakikishia kuwa wataendelea kushirikiana na wananchi katika kuendeleza maendeleo ya kijamii na kuwaomba wapokee msaada huo kwa moyo mkunjufu.

Nao , wananchi waliopatiwa msaada huo wametoa shukrani zao za dhati kwa taasisi hiyo pamoja na Diwani wa Wadi ya Gamba kwa kuwajali na kuwasaidia. Wamesema msaada huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kipindi hiki cha Ramadhani na kuomba kuendelea kupatiwa

ushirikiano katika harakati za maendeleo.
Katika msaada huo, zaidi ya kaya 100 zimepatiwa bidhaa mbalimbali zikiwemo unga wa ngano, tambi, sukari na mafuta ya kupikia kwa ajili ya kujikimu.