Na Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo, amesema serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wote wanaowatumia watoto wadogo katika kazi, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Mhe. Gallos ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa kaskazini Unguja ambapo alieleza kuwa bado kuna changamoto ya uwepo wa ajira za watoto katika mkoa huo licha ya juhudi zinazochukuliwa kupambana na vitendo hivyo.
Amesema kuwa ushirikiano wa wazazi, walezi na viongozi unahitajika ili kudhibiti tatizo hilo, na kusisitiza umuhimu wa kuwapa watoto fursa ya kusoma na kufikia ndoto zao kwa manufaa yao binafsi, familia na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo, na kwamba ipo mipango ya kuunda timu maalum itakayoshughulikia tatizo hilo ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu.
Pia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawahamasisha watoto wao kuzingatia masomo, ili kujenga kizazi bora kitakachochangia maendeleo ya familia na taifa.
