Popular services

DKT. MAHMOUD AELEZA MIKAKATI YA DIVISION ONE TUMBATU, OTHMAN ASISITIZA MAADILI.

 

Tarehe: 7 April 2026
Na: Nishan Khamis, Jimbo la Tumbatu
Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Dkt. Mahmoud Omar Hamad, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali kwa juhudi kubwa za kuimarisha sekta ya elimu katika Jimbo la Tumbatu na Zanzibar kwa ujumla.

Dkt. Mahmoud ameyasema hayo leo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne katika Skuli ya Sekondari Muanda, Wilaya ya Kaskazini A, ambapo alizungumza na walimu, wazazi pamoja na wanafunzi wa skuli hiyo.

Amesema viongozi wa jimbo hilo wamejipanga kuleta mapinduzi ya kimaendeleo katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanafikia ufaulu wa daraja la kwanza, hatua ambayo itasaidia kuzalisha wataalamu na viongozi bora watakaolitumikia taifa siku zijazo.

Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa pamoja kati ya wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na viongozi, akiwataka wadau wote wa elimu kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti itakayoinua kiwango cha ufaulu katika skuli zote za jimbo hilo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimiwa Juma Othman Hija, amewataka wazazi na walimu kuendeleza ushirikiano katika malezi ya watoto kwa kuzingatia maadili mema, ili kuwaepusha na vitendo vya udhalilishaji na mmomonyoko wa maadili. Pia amesisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano, amani na utulivu pamoja na kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoendelea kusimamiwa na viongozi wa kitaifa.

Amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu, kujitambua na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuharibu mustakabali wao. Amesema mafanikio yanahitaji juhudi, uvumilivu na kujituma, hivyo ni muhimu kwa wanafunzi kuweka malengo yao wazi na kuyafuata kwa umakini ili kutimiza ndoto zao za maisha.

Akisoma risala katika mahafali hayo, Mwalimu Arafa Shekhe Khamis amesema jumla ya wanafunzi 71 wamehitimu, ambapo kati yao wanafunzi 22 wamefaulu na kujiunga na kidato cha tano.

Hata hivyo, amebainisha kuwa bado skuli hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, upatikanaji wa umeme pamoja na uhaba wa vifaa katika chumba cha kompyuta. Pamoja na changamoto hizo, Mwalimu Arafa ametoa pongezi za dhati kwa viongozi wa jimbo hilo na wazazi kwa ushirikiano wao mkubwa uliochangia mafanikio ya elimu katika skuli hiyo