Tarehe 7, Aprili 2026 | Nishan Khamis, Kinyasini
Kinyasini, Zanzibar – Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka matawi matatu ya Wilaya ya Bagamoyo wamefanya ziara ya kihistoria katika Tawi la CCM Kinyasini, lililopo Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A, Zanzibar. Ziara hiyo ilihudhuriwa na wanachama wengi na ilidumu zaidi ya siku tatu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Daud Dickinson Kawiche, Mwenyekiti wa CCM Tawi la Majani Mapama, Bagamoyo, alisema kuwa utaratibu huu umefanyika kwa zaidi ya miaka mitano, ambapo matawi ya Bagamoyo huitembelea Zanzibar, na Tawi la CCM Kinyasini huja Bagamoyo. Aliongeza kuwa lengo la ziara hizi ni kuimarisha mshikamano, umoja na undugu kati ya wanachama, huku wakidumisha upendo kwa maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mwenyekiti Daud Dickinson Kawiche alitoa pongezi za dhati kwa marais wote nchini kwa usimamizi mzuri wa ilani ya CCM, ambayo imechangia maendeleo nchini na kuendeleza amani na utulivu. Alisisitiza kuwa wananchi waendelee kutunza tunu hii ya mshikamano, umoja na amani kwa mustakabali wa taifa.
Ziara hii pia ilijumuisha kutembelea maeneo mbalimbali ya kitalii na kihistoria ya Zanzibar, ambapo wanachama walipata fursa ya kujifunza mengi kuhusu historia na utamaduni wa visiwa hivyo.
Kwa upande wao, Khamis Ali Haji, Diwani wa Wadi ya Chaani, na Maimuna Kassim Yussuf, Diwani wa Viti Maalum wa Jimbo la Chaani, walisema kuwa utaratibu wa ziara hizi umeongeza mshikamano wa kisiasa na kijamii kati ya wanachama na ni chachu ya kudumisha mshikamano wa CCM.
Baadhi ya wanachama wa CCM kutoka Bagamoyo na Jimbo la Chaani walisema Ziara hizi zinatufundisha mshikamano na kutufanya tuwe familia moja ya CCM. Tumepata fursa ya kujifunza mengi kuhusu historia ya Zanzibar na kushirikiana katika maendeleo ya chama na taifa.
Ziara hii imeonyesha wazi kuwa mshikamano wa kisiasa una faida kwa wanachama, jamii na taifa, na ni mfano wa kuigwa katika kudumisha umoja wa CCM na Muungano wa Tanzania.
