Popular services

WADI YA CHAANI YAADHIMISHA MIAKA 62 YA MUUNGANO, DIWANI KHAMIS PICHI AWATAKA VIJANA KULINDA TUNU HIYO.

 

Mwandishi: Nishan Khamis, Chaani
Vijana wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuutunza na kudumisha Muungano wa Tanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Wito huo umetolewa leo na Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Pichi, wakati alipojumuika na wanachama wa CCM wa Wadi hiyo katika zoezi la kufanya usafi katika tawi la CCM Chaani Mcheza Shauri, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema vijana wana jukumu kubwa la kulinda tunu ya Muungano kutokana na nafasi yao muhimu katika jamii na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, ametoa pongezi za dhati kwa marais wote wa Tanzania kwa kuendelea kusimamia vyema amani na utulivu, hali inayochangia kudumisha Muungano huo.

Pia ametoa wito kwa vijana na wananchi kwa ujumla kuwaunga mkono viongozi wa nchi ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kupiga hatua za maendeleo, huku akiwataka viongozi wa Jimbo la Chaani kuendeleza umoja na ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wadi ya Chaani, Omar Haji Omar, pamoja na Katibu wa CCM Tawi la Mcheza Shauri, Kijakazi Khamis Salum, wametoa pongezi kwa viongozi wa jimbo hilo kwa ushirikiano wao mkubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Viongozi hao wamesisitiza vijana na jamii kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano katika kulinda na kuenzi Muungano wa Tanzania, huku wakiwataka vijana kuepuka kushawishiwa na watu wenye nia mbaya ya kuuvuruga Muungano huo.

Aidha, wameeleza kuwa wataendelea kuwaunga mkono viongozi wa nchi kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Chaani na Tanzania kwa ujumla.