Na,Nishan khamis, Mkwajuni.
Tarehe 23,April 2026.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Riziki Daniel Yussuf, amewahimiza wanafunzi wa kidato cha sita wa Skuli ya Mkwajuni kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kutumia vyema muda wao ili kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mhe. Riziki amesema kuwa mafanikio katika elimu yanahitaji juhudi binafsi, nidhamu na malengo ya wazi, akisisitiza kuwa hatua wanazochukua leo zitakuwa msingi wa mafanikio yao ya baadaye. Amesema ni muhimu kwa wanafunzi kuepuka vitendo vya udanganyifu katika mitihani, kwani vinaweza kuharibu mustakabali wao wa kielimu.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Ali Mwinyi imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya skuli, upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na mazingira bora kwa wanafunzi. Amesema jitihada hizo zinapaswa kuwa chachu kwa wanafunzi kujituma zaidi ili kufikia ndoto zao.
Mhe. Riziki ameongeza kuwa ofisi ya wilaya itaendelea kusimamia na kuimarisha masuala ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora, huku akitoa wito kwa walimu na wazazi kushirikiana kwa karibu katika kuwaongoza na kuwahamasisha vijana hao kwa maslahi ya taifa. Pia amesisitiza umuhimu wa kuunga mkono juhudi za viongozi wa kitaifa katika kuendeleza elimu ili kuchochea maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Wilaya ya Kaskazini A, Juma Mwadin Abdalla, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa juhudi zake za kuanza kwa kasi katika kuimarisha sekta ya elimu, ikiwemo kukutana na wanafunzi na kuwapa hamasa kuelekea mitihani yao ya taifa. Amesema hatua hiyo imeongeza ari na imani kwa wanafunzi wengi.
Amebainisha kuwa maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya elimu yameleta chachu kubwa kwa wanafunzi kuongeza bidii na nidhamu katika masomo yao, jambo ambalo limeonekana kupitia matokeo mazuri ya kidato cha sita mwaka uliopita. Aidha, ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na walimu na wadau wengine kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kuimarika.
Kwa upande wao wanafunzi wa Skuli ya Mkwajuni wamesema wamefarijika na ujio wa Mkuu wa Wilaya na maelekezo waliyopewa, akieleza kuwa yamewapa motisha mpya ya kusoma kwa bidii na kujiandaa vyema kwa mitihani yao.
Wanafunzi hao wameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ili kufanikisha malengo yao ya kitaaluma na kuchangia maendeleo ya taifa. Pia wametoa shukrani za dhati kwa Rais Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya elimu katika skuli yao, wakisema hatua hiyo imeboresha mazingira ya kujifunzia na kuwapa ari zaidi ya kufanya vizuri.
