NA NISHAN KHAMIS, KASKAZINI UNGUJA
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Cassian Gallos Nyimbo, amewataka wananchi pamoja na wakazi wa mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yanayotarajiwa kufanyika kesho mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, RC Nyimbo amesema Mwenge wa Uhuru utapokelewa kesho kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na kuanza kukimbizwa katika Wilaya ya Kaskazini B.
Amefafanua kuwa Mwenge huo utakimbizwa katika umbali wa kilomita 120, ambapo kilomita 62 ni za Wilaya ya Kaskazini A na kilomita 58 ni za Wilaya ya Kaskazini B.
Aidha, amesema tarehe 12 Mwenge huo utaendelea kukimbizwa katika Wilaya ya Kaskazini A, kabla ya kukabidhiwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam siku ya Jumatatu.
Katika ziara hiyo, jumla ya miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 287,838,543,544.74 itapitiwa, kukaguliwa na kuwekwa mawe ya msingi. Kati ya miradi hiyo, miradi 6 inatoka Kaskazini B na miradi 4 inatoka Kaskazini A.
RC Nyimbo amesisitiza kuwa miradi hiyo inalenga kuimarisha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi, huku akihimiza ushiriki wa wananchi na mikoa jirani katika mapokezi na ushuhudiaji wa shughuli za Mwenge wa Uhuru, akibainisha kuwa ni sehemu ya kuendeleza uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
