Popular services

VIONGOZI WA JIMBO LA MKWAJUNI WAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI KWA WANANCHI.

 VIONGOZI WA JIMBO LA MKWAJUNI WAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI KWA WANANCHI.

Na,Nishan khamis, Mkwajuni.
Viongozi wa Jimbo la Mkwajuni wameendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto ya maji safi na salama inayowakabili wananchi wa maeneo mbalimbali ya jimbo hilo. Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi.

Akizungumza katika moja ya ziara za maendeleo, Mbunge Khamis Ali Vuai na Sulubu Kidongo Amour jimbo la mkwajuni wamesema jumla ya shilingi milioni moja na nusu zimetumika kununulia mipira na vifaa mpaka kukamilika zoezi hilo ambapo wameeleza kuwa suala la maji limepewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya wananchi.

Wamesisitiza kuwa juhudi zaidi zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji kwa urahisi na uhakika pamoja na utatuzi wa changamoto mbali mbali katika jimbo hilo sambamba na kuwahamasisha kuendelea kushirikiana na viongozi na kutunza amani na utulivu nchini.

Katibu wa  siasa chama cha mapinduzi jimbo hilo Juma Mshenga Juma amesema jimbo hilo lipo salama na wataendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM 2025-2030 ili kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza kwa vitendo ahadi na kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni mikakati madhubuti ya chama cha mapinduzi nchini kwa usimamizi bora wa mwenyekiti Dkt Samia Suluhu Hassan na makamo wake Dkt Husein Ali Mwinyi.

Kwa upande wao Wananchi  wamepongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto waliokuwa wakikabiliana nayo hapo awali, hususan kwa kina mama na watoto waliokuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji.